MTANGAZAJI

SERIKALI IJIANDAE KUSULUBIWA TENA BUNGENI

RAIS Jakaya Kikwete alipokuwa akijibu maswali ya wananchi moja kwa moja aliweka bayana kwamba wabunge wana uhuru wa kuikosoa Serikali yake na kwamba kamwe hapendi kuwa sehemu ya wale wanaominya uhuru wa kujieleza. Hata hivyo Kikwete katika matamshi yake siku ile na hata katika hotuba nyingine zilizofuatia anasisitiza kwamba wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi lazima watambue kuwa wana wajibu kwa chama chao.

Kwa tafsiri nyepesi, Rais alikuwa akiwakumbusha wabunge kuwa hakuna haki isiyokuwa na wajibu. 'Wajibu' ni neno ambalo tafsiri yake ni pana kama lilivyo neno 'haki'. Hivyo wale walio watekelezaji wa maagizo ya Rais wanaweza kucheza na maneno hayo kadiri wapendavyo hata kama tafsiri zao hazikidhi kile alichokuwa akijaribu kusema Rais Kikwete.
Mimi ninakuibaliana na kauli ya Kikwete kwamba wabunge wa CCM wanawajibika kwa chama chao ambacho ndiyo tiketi iliyowafikisha bungeni. Hata hivyo wajibu huo kwa chama hauwezi kuwa kipaumbele cha wabunge katika utekelezaji wa majukumu yao ya uwakilishi. Lazima tutambue kwamba licha ya kupitia CCM wabunge hawa walipigiwa kura na wananchi katika maeneo yao.Sifa anazopaswa kuwa nazo mpigarura yoyote Mtanzania hazifungamani na itikadi za kisiasa hata kidogo.


Kwa maana hiyo basi, wapigakura hawalazimiki kuwa wanachama wa vyama vya siasa kama ilivyo kwa wagombea. Hivyo ni dhahiri kwamba wabunge tulionao, wawe ni kutoka chama cha mapinduzi au upinzani wajibu wao wa kwanza ni kwa umma uliowachagua. Wanapaswa kulinda maslahi ya wapigakura wao kwanza kabla ya mambo mengine yoyote.

Hili linaweza kupingwa na yoyote kwa mtazamo wake, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba kwa mwamko wa kisiasa tulionao hivi leo nchini hakuna mbunge au kiongozi mwingine wa kuchaguliwa anayeweza kuwaridhisha wapigakura wake bila kujali maslahi yao. Sasa lile la Rais kwamba wabunge wanawajibika kwa chama chao nalo lina nafasi yake kwa kuzingatia mazingira na mambo mengine kadha wa kadha.

Mathalani, Mbunge wa Ukonga Dk. Millton Mahanga anasimama wapi kuhusu fidia ya wananchi wa Kipawa waliohamishwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege?, James Lembeli, Mbunge wa Kahama anakuwa na msimamo gani dhidi ya fidia kwa wananchi walioathiriwa na ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi? au Ni msimamo gani tunaoutarajia kutoka kwa mbunge wa Ngorongoro, Kaika Saning'o Ole Telele kuhusu wananchi wa Loliondo waliochomewa nyumba zao?


Wabunge hawa na wengine ambao sikuwataja ni dhahiri kwamba wataegemea upande wa wale wanaowawakilisha wakitaka Serikali inayoongozwa na chama kilichowapa tiketi za kuingia bungeni ichukue hatua dhidi ya matatizo haya. Hata kama ni kuondoa shilingi kwenye makadirio ya bajeti ya wizara fualani basi watafanya hivyo na hiyo ndiyo kazi yao.

Kwa upande mwingine yapo maamuzi ya bunge ambayo hufikiwa kwa mujibu wa kanuni za bunge. Katika bunge la Tanzania wabunge wa chama tawala ni wengi kwa idadi hivyo maamuzi mengi huzingatia matakwa ya chama chao hata kama wapinzani wasingependa yapite. Mfano halisi ni bajeti kuu ya Serikali ambayo hata wapinzani waipinge vipi, hupita kutokana na wingi wa wabunge wa chama tawala.

Kutokana na utamaduni huu wa chama tawala kupitisha maamuzi kutokana na wingi wa wabunge wake, hivi sasa Serikali ni kama imekuwa ikijisahau na kudhani kuwa kila uamuzi wake ni lazima ukubaliwe na wabunge hata kama hauna maslahi kwa umma. Mfano halisini suala la Richmond ambalo lilileta mvutano mkubwa baina ya Serikali na bunge kiasi cha Spika Samuel Sitta kuingilia kati kuokoa jahazi. Hakuwa rahis kama watendaji Serikalini walivyodhani kwamba wabunge wangeweza kuridhika kuwa hakukuwa na wakosaji katika mlolongo mzima ulioipa ushindi wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kampuni hiyo ya Richmond.

Hapa tuliwaona wabunge wa CCM na wale wa upinzani wakiungana na kuwa kitu kimoja. Ile hoja kwamba maazimio ya bunge yalitekelezwa ikalala kiporo na sasa inasubiri utekelezaji mpya ambao taarifa yake lazima iwasilishwe katika kikao cha Bunge kinachotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Wakati hilo likisubiriwa kwa hamu ni dhahiri kwamba serikali huenda ikajikuta katika wakati mgumu kufuatia kusaini mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Kuhudumia Kontena Bandarini (TICTS) ya kuondoa kipengele cha ukiritimba pekee katika mkataba na kampuni hiyo. Hatua hiyo ni tofauti na msimamo wa wabunge wengi ambao walikuwa wakitaka ama kuvunjwa kwa mkataba huo au kufupishwa kwa muda wa mkataba huo wa Ticts ambao uliongezewa miaka 15 zaidi kinyemela.

Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Godfrey Zambi juzialinukuliwa na KULIKONI akisema kuwa “Kimsingi Serikali imepuuza maazimio ya Bunge kuhusu Ticts kwa sababu Bunge liliagiza kushughulikiwa kwa mambo mawili lakini wao wameshughulikia jambo moja tu.”

Zambi ndiye aliyewasilisha bungeni hoja ya kutaka kuvunjwa kwa mkataba huo kutokana na kuongezwa kinyemela kwa miaka 15 zaidi tofauti na ile iliyokuwa imefikiwa katika mkataba wa awali ambao ulitakiwa kumalizika mwaka 2010. Kwa mujibu wa Zambi suala la kupunguza muda wa miaka 15 ulioongezwa kinyemela Serikali haikulifanyia kazi kabisa na kwamba ana ushahidi kwa sababu nyaraka zote za vikao vya mawaziri ambazo zinathibitisha suala la kufutwa kwa miaka 15 ya nyongeza halikuwa sehemu ya majadiliano hayo.

Kwa mujibu wa mbunge huyo mkataba huo ungeweza kuvunjwa hata bila serikali kupata hasara kwani Ticts walikuwa wakifanya kazi chini kiwango cha makubaliano na kwamba mkataba huo unaruhusu Serikali kuuvuja inapotokea hali ya namba hiyo.

Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa aliwaambia waandishi wa habari baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kuondoa ukiritimba wa Ticts kuwa: “Tumejadiliana kwa muda mrefu na wenzetu hawa TICTS wamekubali kuendelea na mkataba wao wa miaka 25 bila kipengele hicho na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenzao kwa ajili ya kuboresha ufanisi katika bandari yetu.”

Kwa kauli hiyo ya Dk. Kawambwa ni dhahiri Ticts wanaendelea na mkataba wao kwa miaka 15 ijayo licha ya kwamba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliwahi kupendekeza kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuishawishi serikali kuuvunja mkataba huo mara moja.

Kadhalika, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwahi kuliambia Bunge kuwa mkataba kati ya Serikali TICTS) ni bora uvunjwe kwa gharama yoyote kwa sababu imeshindwa kazi na kunahitajika ushindani ili kuongeza ufanisi katika bandari hiyo. Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni Waziri Mkuu alikiri mkataba huo wa TICTS kuongezwa bila kuzingatia mazingira ya wakati huo, lakini sasa imegundulika kuwa kampuni hiyo imeshindwa kazi.

Kwa hakika huu ni uchokozi mwingine wa Serikali kwa Bunge na wabunge. Katika hali ya upuuzaji wa maazimio ya bunge kwa kiwango hiki ni lazima tujue kuwa kile kinachoonekana kuwa ni 'utovu wa nidhamu' wa wabunge hasa wa CCM mbele ya serikali yao lazima utaendelea. Utaendelea tu kwa sababu Serikali inapenda sana wabunge wawajibike kwa kutoishambulia lakini wao (Serikalini) ni wazito kutekeleza yalioyo maazimio ya umma yanayofikiwa kupitia vikao halali vya bunge.

Kinachoonekana katika hili la Ticts ni kama Serikali inathamini sana matakwa ya kampuni hii kuliko matakwa ya wananchi kupitia wabunge wao. Katika hali hii ni kwamba Serikali ijiandae kusulubiwa tena bungeni maana wabunge hawawezi kukubali. Hatuwezi kuendelea katika hali hii na kwa hili lazima serikali IJISAHIHISHE…..

Neville Meena ,Mhariri Msaidizi wa Kulikoni Simu: 078 7675555,
barua pepe: nevilletz@yahoo.com

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.