MTANGAZAJI

SERA MPYA INAYOWAHUSU WAHAMIAJI HOUSTON, MAREKANI

 


Jiji la Houston nchini Marekani limeanza kutekeleza sera mpya ya kupunguza ushirikiano kati ya Polisi wa Houston, Texas  na Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani, maarufu kama ICE.

Meya wa Houston, John Whitmire, ametangaza kuwa polisi wa jiji hilo watawasiliana na ICE tu pale mtu atakapokamatwa kwa kosa linaloweza kusababisha kifungo jela au ikiwa maafisa wa uhamiaji wametoa hati rasmi ya kumtafuta mtu huyo.

Tangazo hilo limekuja kufuatia mabadiliko  ya kisiasa katika jimbo Texas baada ya ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa kati ya muhula nchini Marekani wa hivi karibuni, ikiwemo ushindi wa Gina Hinojosa dhidi ya Greg Abbott katika uchaguzi wa ugavana.

Houston imeendelea kuwa moja ya miji yenye idadi kubwa ya wahamiaji nchini Marekani. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa eneo la Houston lina zaidi ya wahamiaji milioni 1.6, sawa na takribani robo moja ya wakazi wote wa eneo hilo.idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 32 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita

Wahamiaji wengi wanaoishi Houston wanatoka Mexico, India, Vietnam, El Salvador, Honduras, Venezuela, Guatemala, Cuba, Ufilipino na Colombia, huku jamii za Kiafrika nazo zikiendelea kukua kwa kasi, ikiwemo kutoka Nigeria, Cameroon, Ethiopia, Ghana, Kenya,Tanzania,DRC na Uganda. 

Takwimu za Taasisi ya Uhamiaji na Sera (MPI) zinaonesha kuwa  wahamiaji ni sehemu muhimu ya ukuaji wa Houston kutokana na mchango wao katika soko la ajira, biashara na mapato ya kodi. Wahamiaji hao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika sekta za afya, ujenzi, usafirishaji, nishati na huduma nyingine muhimu, huku  wakiongeza matumizi ya bidhaa na huduma na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa jiji hilo. 

Kwa mujibu wa viongozi wa jiji, lengo la sera hiyo ni kuhakikisha wahamiaji wanaofuata sheria hawana hofu ya kusimamishwa na polisi wanapokwenda kazini, shuleni au kutafuta huduma muhimu.

Hata hivyo, ICE imepinga uamuzi huo ikisema unapunguza ushirikiano muhimu wa vyombo vya usalama katika kutekeleza sheria za uhamiaji na kulinda jamii.

Wanaharakati wa haki za wahamiaji jijini Houston wamepongeza hatua hiyo wakisema itasaidia kurejesha imani kati ya wahamiaji na vyombo vya usalama.

Sera hiyo mpya inakuja wakati mjadala kuhusu uhamiaji ukiendelea kushika nchini Marekani, hasa baada ya uchaguzi wa hivi karibuni katika jimbo la Texas.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.