MFAHAMU KIONGOZI WA KANISA LA WAADVENTISTA WA SABATO ECD
Wakati wa mchakato wa uchaguzi, Kamati Kuu ya Utendaji ya ECD ilibainisha vipaumbele kadhaa kwa mwenyekiti wake ajaye, ikiwemo uadilifu, uongozi wa kiroho, shauku ya utume, na uwezo wa kuwaleta watu pamoja. Kamati hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa kuandaa viongozi wa baadaye, kuelewa tamaduni mbalimbali ndani ya divisheni hiyo yenye nchi 11, na kuimarisha uwezo wa kanisa kuunga mkono utume wake.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo ulimwenguni, Erton C. Köhler, alisisitiza umuhimu wa uongozi unaomweka Kristo katikati na kubaki makini katika utume wa kanisa.
“Kiongozi katika kanisa, kwanza kabisa, ameitwa kumtumikia Mungu na watu Wake. Wakati Mchungaji Maka anapochukua jukumu hili jipya, ombi langu ni kwamba ataendelea kuongoza kwa unyenyekevu, ujasiri, na kujitoa kwa dhati katika utume,” alisema Köhler. “Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati ina fursa kubwa za kuwafikia watu kwa ajili ya Kristo, na ni lazima tubaki na umoja, tukiwa tumejengwa juu ya Biblia na kuendelea kuzingatia utume ambao Mungu ametukabidhi.”
Mzaliwa wa Buwagi, Jinja, Uganda mwaka 1969, Maka alipata Shahada ya Kwanza ya Thiolojia katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha Spicer nchini India, kabla ya kukamilisha Shahada ya Uzamili ya Thiolojia katika Chuo cha Newbold nchini Uingereza na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Thiolojia na Ufafanuzi wa Agano la Kale kutoka Chuo Kikuu cha Sahmyook nchini Korea Kusini.
Akiwa mchungaji aliyewekwa wakfu, Maka alianza kulitumikia Kanisa la Waadventista wa Sabato mwaka 1995. Katika huduma yake, amewahi kuhudumu kwa nafasi ya mchungaji, kiongozi wa mtaa(kanisa), mhadhiri, na Kiongozi katika nafasi kadhaa za kanisa ikiwemo Chuo Kikuu cha Bugema.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa ECD, Maka alikuwa Mwenyekiti wa Unioni Misheni ya Uganda ambako alishawahi kuwa Katibu Mtendaji. Katika kipindi cha uongozi wake, alianzisha maeneo matano mapya ya kiutawala ndani ya unioni hiyo. Huduma yake pia imejumuisha uinjilisti, ulezi wa kiroho, na kuanzisha makanisa mapya.
Maka ameoana na Janet Maka, na wamebarikiwa watoto wanne.
.png)
Post a Comment