KESI YA HAKI MILIKI DHIDI YA WAADVENTISTA YATUPILIWA MBALI.
Jaji wa shirikisho huko Tennessee, Marekani ametupilia mbali kesi iliyofunguliwa na mtunzi wa muziki Brian Sitler dhidi ya Kituo cha Vijana cha Uinjilisti (CYE) na mashirika mengine matatu ya Waadventista kuhusu muziki uliotengenezwa kwa ajili ya Kamporii ya Kimataifa ya Watafuta njia ya mwaka 2019.
Sitler alidai kuwa muziki alioutengeneza kwa makubaliano ya mwaka 2015 uliendelea kusambazwa na kutumika baada ya tukio la mwaka 2019 bila kibali chake, ikiwemo katika Kamporii ya mwaka 2024.
Katika uamuzi wa Novemba 16, mwaka huu Jaji wa Mahakama ya Wilaya nchini Marekani, Eli Richardson, alitupilia mbali madai yote ya Sitler kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama ya Wilaya.
Sitler alifungua kesi dhidi ya CYE, Chuo Kikuu cha Andrews (AU), Hope Channel International na AdventSource. Mahakama ilitupilia mbali madai ya ukiukaji wa hakimiliki dhidi ya AU, Hope Channel na AdventSource kwa sababu Sitler hakuthibitisha kuwa mahakama ya Tennessee ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi dhidi ya mashirika hayo.
Kutupiliwa mbali kwa madai hayo hakukuamua iwapo kulikuwa na ukiukaji wa hakimiliki au la. Mahakama pia ilitupilia mbali dai la uvunjaji wa mkataba dhidi ya CYE kwa kuwa makubaliano ya mwaka 2015 yalifanywa na kampuni ya uzalishaji ya Sitler, si yeye binafsi. Vilevile, dai lake la hakimiliki dhidi ya kituo hicho lilitupiliwa mbali baada ya jaji kubaini kuwa majibu yake hayakujibu ipasavyo hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi.
Kesi hiyo ilihusu muziki uliotengenezwa kwa ajili ya Kamporii ya Kimataifa ya Watafuta njia, moja ya matukio makubwa zaidi ya vijana ndani ya Kanisa la Waadventista wa Sabato duniani. Zaidi ya watu 55,000 walihudhuria Kamporii ya mwaka 2019 huko Oshkosh, Wisconsin. Tukio la mwaka 2024 lilifanyika Gillette, Wyoming, na kuwakusanya zaidi ya Watafuta njia na wafuasi 60,000 kutoka zaidi ya nchi 100.
Kamporii ijayo itafanyika Oshkosh mwaka 2029 kupitia kaulimbiu ya “Simama Imara", itakayofanyika Agosti 20 hadi 26 katika viwanja vya Experimental Aircraft Association.

.png)
Post a Comment