MTANGAZAJI

ALIYEKUWA AFISA WA UHAMIAJI ATUHUMIWA KUPOKEA RUSHWA ZA WAHAMIAJI MAREKANI.


Afisa wa zamani wa Idara ya Uhamiaji nchini Marekani,(USCIS) amekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kuuza hadhi na vitambulisho vya ukaazi halali wa kudumu kwa wahamiaji nchini humo maarufu green cards.

Lukman Owolabi Ganiyu alikamatwa Septemba 2, baada ya uchunguzi wa miaka kadhaa kuonyesha kuwa kati ya mwaka 2019 na 2026 alitumia nafasi yake ndani ya USCIS kuidhinisha maombi ya uhamiaji kwa malipo ya fedha. Waendesha mashtaka wanasema aliidhinisha maombi ya ukaaji wa kudumu, udhamini wa kifamilia, kuondoa masharti ya ukaaji, na hata kuidhinisha uraia, bila kufuata taratibu za lazima za serikali ya Marekani.
 
Kwa mujibu wa hati ya kiapo, uchunguzi ulibaini zaidi ya dola za Marekani 287,000 zilizowekwa kwenye akaunti zake za benki bila maelezo, pamoja na zaidi ya dola 671,000 zilizolipwa kupitia Zelle, Cash App na majukwaa mengine. Baadhi ya malipo hayo yalihusishwa moja kwa moja na waombaji wa Idara ya Uhamiaji. Ganiyu, ambaye alipata takribani dola 407,000 kama mshahara kati ya 2020 na 2025, hakuwa na ajira nyingine nje ya serikali.
 
 Mwendesha Mashtaka wa Marekani wa Kaskazini mwa Jimbo la Texas,  Ryan Raybould, ametangaza kwamba Ganiyu alishirikiana na Adeniyi Akeem Somoye, ambaye pia amekamatwa. Mawasiliano yao ya WhatsApp yanadaiwa kuonyesha mipango ya kukusanya mamia ya maelfu ya dola kutoka kwa waombaji. Uchunguzi unaonyesha Ganiyu alijipangia kushughulikia maombi ya uraia ya Somoye na kuyaidhinisha siku hiyo hiyo mnamo Desemba 2022, kisha kupokea zaidi ya dola 138,000 kutoka kwa Somoye katika kipindi cha miaka mitatu.
 
Uchunguzi ulianza Mei 2025 baada ya USCIS kupokea taarifa kwamba Ganiyu alikuwa anachanganua na kushughulikia maombi fulani nje ya utaratibu. Barua pepe zake za serikali zilionyesha rekodi za benki na malipo kutoka kwa Somoye. Ganiyu alijiuzulu Machi 21 mwaka huu kwa madai ya sababu binafsi.
 
Waendesha mashtaka wanasema Ganiyu hakushughulikia mahojiano ya lazima, ukaguzi wa wasimamizi, ukaguzi wa historia ya waombaji na taratibu nyingine za usalama, na kwamba baadhi ya waombaji aliowasaidia hawakuwa na sifa za kupata manufaa ya uhamiaji.
 
Mwendesha Mashtaka, Ryan Raybould, amesema “Kuuza manufaa ya uhamiaji ni usaliti wa wazi kwa umma, na hatutavumilia rushwa katika eneo letu.” USCIS pia imesema hakuna nafasi ya matumizi mabaya ya madaraka ndani ya taasisi hiyo.
 
Kesi hii inachunguzwa na USCIS, Ofisi ya Idara ya Usalama wa Ndani(DHS), na FBI. Waendesha mashtaka waliotaka Ganiyu azuiliwe kutokana na uraia wake wa Nigeria na Marekani na mali alizonazo nje ya Marekani, lakini hakimu ameamuru aachiwe kwa masharti maalum, ikiwemo ufuatiliwaji wa GPS na kukabidhi pasi zake za kusafiria.
 
Ikiwa watapatikana na hatia, Ganiyu na Somoye wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 5 na faini ya hadi dola 250,000 kila mmoja.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.