MTANGAZAJI

MATUMIZI YA LESENI YA UDEREVA YA KIDIJITALI

 

Katika dunia ya sasa ambapo simu janja zimekuwa kiungo muhimu cha maisha ya kila siku, serikali na taasisi mbalimbali zimeanza kuhamisha huduma muhimu kwenda kwenye mifumo ya kidijitali. Mojawapo ya mageuzi makubwa katika eneo hili ni Leseni ya udereva ya kidijitali(mDL) inayohifadhiwa salama kwenye simu ya kiganjani.
 
mDL ni moja ya mageuzi makubwa katika utambuzi wa kitambulisho cha kidijitali, ni teknolojia inayobadilisha namna tunavyobeba na kuwasilisha leseni za udereva. 
Wazo la mDL lilianza kuchukua sura mpya mwaka 2010 wakati juhudi za kuhamisha hati muhimu za serikali nchini Marekani kwenda kwenye mifumo ya kidijitali zilipoanza kushika kasi. 
 
Mwaka 2018,  jimbo  Louisiana nchini Marekani lilikuwa miongoni mwa waanzilishi kupitia programu ya LA Wallet, lakini mDL ya kisasa ilipata umaarufu mkubwa mwaka 2021 baada ya kampuni Apple kushirikiana na jimbo ya Arizona kuwezesha leseni ya kidijitali ndani ya Apple Wallet. 
 
Baadaye, Google na Samsung walijiunga katika kuendeleza teknolojia hii, huku Shirika la Viwango Duniani (ISO) likitoa kiwango cha ISO 18013-5 kinachoweka viwango vya usalama na uoanifu wa kimataifa.
 
 Kufikia mwaka 2026, zaidi ya majimbo 20 nchini Marekani yanatoa mDL na Mamlaka ya Usalama wa Usafiri nchini Marekani (TSA), maarufu kwa ukaguzi wa abiria kwenye viwanja vya ndege imeanza kukubali matumizi ya mDL katika viwanja vingi vya ndege, jambo lililorahisisha usafiri na uthibitishaji wa kitambulisho hasa baada ya utekelezaji wa sheria ya mpango wa serikali ya Marekani unaoweka viwango vya kitaifa vya usalama kwa vitambulisho vya serikali ikiwemo leseni ya udereva na kitambulisho cha ukaazi cha jimbo, lengo lake ni kuhakikisha kuwa vitambulisho vinavyotumiwa kwa shughuli nyeti hasa kusafiri kwa ndege ndani ya Marekani vinakuwa na kiwango cha juu cha uthibitishaji na ulinzi dhidi ya wizi wa kitambulisho
 
Teknolojia hii inatoa faida nyingi, ikiwemo uwezo wa kushiriki taarifa chache tu unapohitajika, kupunguza hatari ya wizi wa kitambulisho, na kurahisisha ukaguzi wa usalama ukilinganisha na leseni ya karatasi au plastiki. Inapunguza hatari ya wizi wa kitambulisho kwa sababu taarifa zako hazihifadhiwi wazi  zinatunzwa kwa usimbaji fiche ndani ya simu yako. mDL ina uwezo wa kushiriki taarifa maalum pekee, kwa mfano, unaweza kuthibitisha umri wako bila kuonyesha anwani au namba ya leseni, jambo linalolinda faragha yako. Uthibitishaji wake ni wa kidijitali, hivyo ni vigumu kughushi au kutumia leseni ya mtu mwingine. 
 
mDL ina ulinzi wa uthibitishaji wa uso au alama ya kidole, kuhakikisha ni mmiliki halali pekee anayeweza kuitumia.
 
Kwa sasa Simu zinazotumia teknolojia kuwezesha mDL ni pamoja ni kuanzia  iPhone 8 na matoleo mapya zaidi yenye iOS 15.4 au juu, pamoja na saa janja za Apple katika baadhi ya maeneo. Kwa upande wa Android, Google Wallet inahitaji Android toleo la 9 au juu na simu zenye NFC ikiwemo  Google Pixel, Samsung Galaxy, OnePlus na Motorola. Samsung Wallet pia imeanza kutumika katika majimbo kadhaa ikiwemo California. 
 
Nchi zinazoitambua mDL kwa sasa ni Marekani ikiwa ni  kinara kwa kuwa na  watumiaji takribani milioni 5, huku Ulaya na Australia zikiwa na mifumo ya kitambulisho cha kidijitali (digital ID) inayokua ingawa si yote inayolingana moja kwa moja na mDL ya Marekani. 
 
Kwa ujumla, mDL inaonekana kuwa mustakabali wa kitambulisho cha kidijitali salama, rahisi, na rafiki kwa mazingira na watumiaji wanaoishi Marekani au wanaosafiri mara kwa mara wanahimizwa kuangalia kama majimbo yao yanatoa huduma hii na kuanza kuitumia. 
 
Hata hivyo, bado inashauriwa kubeba leseni halisi katika baadhi ya shughuli za kiserikali na safari.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.