MTANGAZAJI

TAMKO LA WAADVENTISTA KENYA KUHUSU UTAPELI WA CRYPTO

 


Mimi ni Mchungaji  Samuel Misiani, Mwenyekiti wa Unioni Konferensi  ya Magharibi ya Kenya ya Kanisa la Waadventista wa Sabato,  pia kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Kenya kwa mujibu wa nafasi yangu.  Kwa niaba ya uongozi wa  Unioni Konferensi ya Magharibi ya Kenya na Unioni Konferensi ya Mashariki mwa Kenya tungependa kushughulikia wasiwasi uliotokana na shughuli zinazohusishwa na mpango wa uwekezaji unaoitwa Opticoin Wealth Sharing Group. 

Kuna taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya watu, wakiwemo washiriki na viongozi fulani wa Kanisa, huenda walishiriki na/au walihusishwa katika kutangaza mpango wa Opticoin Wealth Sharing Group, ambao una sifa zinazofanana na  mifumo ya Piramidi au Ponzi

Kwa kuzingatia wasiwasi huu, tungependa kufafanua yafuatayo:

Mosi 

 Kanisa la Waadventista wa Sabato halimiliki, halikubali, halidhamini, halitangazi, wala haliruhusu mpango wowote wa piramidi, mpango wa Ponzi, mpango wa uwekezaji wa udanganyifu, au biashara yoyote ya kifedha isiyodhibitiwa. Kanisa halikuwa sehemu ya Opticoin Wealth Sharing Group, na halijawahi kuhusishwa na shughuli zake kwa namna yoyote ile.

Pili

Biashara au shughuli yoyote ya kifedha inayofanywa na mshiriki, mfanyakazi, mchungaji, afisa, au kiongozi katika uwezo wao binafsi haiwakilishi  shughuli rasmi, huduma, au msimamo wa Kanisa. Ushiriki wa mtu binafsi katika Opticoin Wealth Sharing Group ulifanywa kwa uwezo binafsi, bila mamlaka, idhini, au agizo la Kanisa.

 Kwa hivyo, ingawa Kanisa linaonesha masikitiko kwa wale waliopata hasara au matatizo, halitambui jukumu la kisheria, kifedha, au la taasisi kwa hasara zilizotokana na ushiriki katika mpango huo. Kanisa linawashauri kwa msisitizo washiriki na umma kuepuka mipango ya kifedha inayotoa ahadi za faida zisizo halisi au zilizohakikishwa, inayotegemea zaidi uandikishaji wa watu wapya, isiyo na udhibiti wa kisheria, isiyo na uwazi au uwajibikaji, au inayoweza kusababisha hasara ya kifedha kwa watu na familia.

Tunatambua kwa masikitiko makubwa dhiki, matatizo, na hasara ambazo watu na familia wamepitia. Kanisa halikubali  unyonyaji, udanganyifu, matumizi mabaya ya ushawishi, au matumizi mabaya ya mamlaka ya kiroho kwa faida binafsi.

 Wakati huohuo, tumejitolea kutoa faraja ya kiroho, huduma ya kichungaji, na maombi kwa wote walioathirika katika kipindi hiki kigumu.Kanisa la Waadventista wa Sabato linadumisha kanuni ya kibiblia ya heshima ya kazi ya uaminifu. Tunaamini kuwa kazi imewekwa na Mungu, na ina mizizi katika uumbaji na katika mpango wa ukombozi. 

Maandiko yanafundisha kuwa Mungu aliumba dunia kwa siku sita halisi na akapumzika siku ya saba, na hivyo akamwagiza mwanadamu kufanya kazi kwa siku sita na kupumzika Sabato kulingana na amri yake. Amri ya nne inathibitisha heshima na thamani ya kazi ya uaminifu.Biblia pia inafundisha kwamba “asiyetaka kufanya kazi, na asile.” 

Mila na desturi zinazohamasisha mipango ya kupata utajiri wa haraka hazipatani na kanuni za Mungu za bidii, uadilifu, uwakili, na kazi ya uaminifu.Kazi yoyote halali na ya uaminifu inayofanywa kwa uadilifu ni ya heshima mbele za Mungu na ni yenye manufaa kwa jamii.

 Kwa hiyo, tunawahimiza washiriki wetu wote waweke tumaini lao kwa Mungu, wajihusishe na kazi ya uaminifu na ya maadili, na kudumisha maadili ya kibiblia katika shughuli zote za kifedha.Tunawasihi washiriki wetu wabaki imara katika Maandiko, wakilenga utume wa Kanisa, na wawe waangalifu dhidi ya ushawishi na desturi zinazoweza kupelekea uharibifu wa kiroho, kimaadili, na kifedha.

 Mungu awape watu wake hekima, utambuzi, na uaminifu. 

Asanteni.

 

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.