NYOTA WA NBA AJAYE ALIYESHAWISHIWA NA DEREVA WA BODA BODA
Khaman Maluach, kijana kutoka Sudan Kusini, ameweka historia mpya baada ya kuchaguliwa katika Draft ya NBA ( wachezaji wa ligi kuu ya mpira wa kikapu nchini Marekani) mwaka 2025 akiwa na umri wa miaka 18 tu. Alichaguliwa kama chaguo la 10 na Houston Rockets ya Texas, lakini kwa mchakato wa kubadilishana wachezaji,sasa amejiunga rasmi na Phoenix Suns ya Arizona, Marekani.
Vyanzo vya habari za NBA vinaeleza kuwa Maluach anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya jumla ya karibu dola milioni 23 hadi milioni 25, huku kwa mwaka wa kwanza akitaraji kupata takribani dola milioni 6.1
Draft ya NBA 2025 ilifanyika Juni 25 hadi 26 mwaka huu katika ukumbi wa Barclays Center ulioko Brooklyn, New York. Tukio hili lilirushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya ABC na ESPN, pamoja na programu tumishi ya ESPN kwa njia ya mtandao. Raundi ya kwanza ilifanyika Juni 25 kuanzia saa mbili usiku kwa saa za mashariki za Marekani, huku raundi ya pili ikifanyika siku iliyofuata, Juni 26 muda huo huo.
Radio ya ESPN nayo ilitoa matangazo ya radio ya moja kwa moja. Ingawa NBA haikutoa idadi rasmi ya watazamaji waliokuwepo ukumbini, inakadiriwa kuwa ukumbi wa Barclays Center unaweza kuchukua hadi watu 17,000, hivyo tukio hilo lilihudhuriwa na maelfu ya watu. Takwimu za mtandao wa Front Office Sport zinaonesha kuwa Raundi ya kwanza ya NBA Draft 2025 ilivutia watazamaji wanaokadiliwa kuwa milioni 3.77 kupitia ABC na ESPN, ikiwa ni punguzo la 14.5% ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilikuwa takriban 4.41 milioni.
Khaman alizaliwa Septemba 14, 2006 huko Rumbek, Sudan Kusini. Baada ya familia yake kukimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, walihamia Uganda, ambako aligunduliwa na dereva wa boda boda aliyemshawishi acheze mchezo wa mpira wa kikapu kutokana na kimo chake na kupelekwa kwenye kambi ya mafunzo iliyoasisiwa na nyota wa zamani wa NBA, Luol Deng mwenye asili ya nchi ya Sudan Kusini.
Kupitia juhudi zake, Khaman alichaguliwa kujiunga na Academy ya NBA Africa iliyoko Dakar, Senegal,mwaka 2021, na hapo ndipo ndoto yake ya kuwa mchezaji wa kimataifa ilipoanza kutimia.
Uchezaji wake mzuri mzuri katika Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika pamoja na kutunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) katika kambi ya Mchezo wa Kikapu usio na Mipaka Afrika ya mwaka 2023 vilithibitisha hadhi yake kama mchezaji mwenye vipaji vya juu, na alikubali kujiunga na timu ya Chuo Kikuu cha Duke kilichopo Durham, North Carolina.
Takwimu zake za mwaka wa kwanza akiwa Chuo Kikuu cha Duke, Marekani 2024-2025.
Pointi kwa mchezo: 8.4
Rebounds: 5.3
Block shots: 1.9
Field Goal %: 79.2%
Free Throw %: 80.0%
Michezo aliyocheza: 32
Dakika kwa mchezo: 18.2
Double-doubles: 4
Blocks nyingi zaidi kwa mchezo mmoja: 6
Tuzo: Amewahi kutajwa Rookie wa juma mara 2 katika ligi ya Chuo Kikuu.
Khaman aliiwakilisha Sudan Kusini kwenye Kombe la Dunia la Mpira wa Kikapu (FIBA) mwaka 2023, akiwa na umri wa miaka 16 tu mmoja wa wachezaji wachanga zaidi kuwahi kushiriki mashindano hayo. Pia alishiriki kwenye Michezo ya Olimpiki Paris 2024, akiendeleza heshima kwa taifa lake.
Familia ya Maluach ilikuwa imepanga kuwepo kwenye tukio la Draft ya NBA 2025 , lakini maombi yao ya visa yalikataliwa kutokana na marufuku ya kuingia Marekani inayowaathiri raia wa Sudan Kusini.
Ni dada yake tu, Agum Madit, ambaye anaishi Australia, ndiye aliyeweza kuhudhuria tukio hilo huko New York.
Kocha wa Maluach kutoka Solid Skills Academy mjini Kampala,Uganda ambayo ndio iligundua kipaji chake kwa mara ya kwanza, naye pia alitarajiwa kuwepo.
"Hiyo ilikuwa bahati mbaya sana. Imeondoa sehemu ya furaha yetu," kocha Wal Deng aliviambia vyombo vya habari."Lakini hata hivyo, tunajivunia sana kwake.
"Ni kama ndoto ambayo imekuwa halisi. Kuona ametoka mbali kiasi gani, kutoka kujifunza misingi ya mpira wa kikapu hadi sasa kujiunga na NBA, huu ni wakati wa furaha kubwa sana."
Hali ya Maluach nchini Marekani sasa inaonekana kuwa salama.Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Duke, alipata visa ya F1, ambayo ni visa ya kawaida ya mwanafunzi nchini Marekani, lakini baadaye ilisitishwa kwa raia wa Sudan Kusini mnamo Aprili. Visa hiyo ya F1 tayari ilikuwa imebadilishwa kuwa visa ya watalii wakati Maluach akisubiri Draft ya NBA.
Sasa akiwa amechaguliwa rasmi kwenye Draft, atahamia kwenye visa ya P1, ambayo kawaida hutolewa kwa wanamichezo wa kulipwa wanaoshiriki kwenye ligi kubwa za Marekani.
Wachezaji wengi wa kimataifa wa NBA hubaki na visa ya P1 kwa muda wote wa kazi zao.
Kocha wake wa chuo, Jon Scheyer, amesema Khaman ana akili ya mchezo na urefu unaomruhusu kutawala mchezo. Ana uwezo wa kipekee wa kulinda, kuruka, na kupiga block kwa wepesi mkubwa ni mchezaji wa aina ya nadra.”
Khaman Maluach sasa ni miongoni mwa wachezaji wa Kiafrika wanaotarajiwa kuwa nyota wakubwa wa baadaye katika NBA. Safari yake imekuwa mfano halisi wa ushindi wa ndoto dhidi ya vikwazo, na sauti yake inasikika kwa vijana wote wa Afrika “Inawezekana.”
Post a Comment