DAKTARI AFARIKI WAKATI AKIMWOKOA ALIYETAKA KUZAMA
Dr.Zhang Junqiao alifariki Juni 25,2025 huko Kigamboni jijini Dar es salaam, Tanzania baada ya kuzama majini wakati akimuokoa mwananchi aliyekuwa anazama.
Siku ya tukio Dr. Zhang alimuona mwananchi akizama na yeye kuamua kujitosa majini kumuokoa. Alipomfikia alimpatia jaketi lake la kuogelea na yeye kwa kuwa ni mzoefu akaogelea bila jaketi. Raia aliyekua akizama alifanikiwa kuokolewa, lakini maji yalimzidi nguvu Dr. Zhang akazama na kupoteza maisha.
Dr.Zhang alikuwa daktari Bingwa wa Dawa za Usingizi na Ganzi, raia wa China aliyekuwa anafanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.
Dr.Zhang alikua na Shahada ya daktari wa binadamu,Shahada ya upasuaji, Shahada ya umahiri katika matibabu ya ndani na Shahada ya umahiri katika dawa za usingizi.
Pia alikua na cheti cha Ithibati ya kimataifa cha kuhudumu kama daktari bingwa wa dawa za usingizi katika nchi zaidi ya 100 duniani (NMLE).
Dr.Zhang atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuhudumia jamii ya watanzania, pamoja na umahiri wake kufundisha njia mpya za dawa za usingizi na ganzi. Atakumbukwa pia kwa ucheshi wake, uchangamfu wake na ari yake katika kazi. Dr.Zhang amepoteza maisha kishujaa akijaribu kuokoa maisha ya Mtanzania mwenzetu aliyekua akizama.
Huu ni upendo wa ajabu. Dr.Zhang amefariki akiwa na umri wa miaka 38.
Credit: Boniphace Anajus
Post a Comment