MAREKANI YAPUNGUZA VITUO VYA VISA AFRIKA.
Serikali ya Marekani imepanga kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utoaji visa barani Afrika kwa kupunguza idadi ya balozi na ofisi za ubalozi zinazoshughulikia maombi ya visa. Hatua hiyo inatarajiwa kuathiri maelfu ya Waafrika wanaotaka kusafiri kwenda Marekani kwa sababu mbalimbali zikiwemo masomo, biashara, utalii na uhamiaji.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Associated Press (AP), karibu vituo 50 vya Marekani vilivyokuwa vikitoa huduma za visa barani Afrika vitapunguzwa na kubaki vituo 20 pekee katika siku chache zijazo.
Sababu za Mabadiliko Haya
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa utawala wa Rais Donald Trump wa kuimarisha udhibiti wa uhamiaji nchini Marekani. Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa visa zinatolewa kwa umakini mkubwa zaidi na kuzuia visa kutumiwa vibaya na watu wanaoingia nchini humo kwa vibali vya muda kisha kubaki zaidi ya muda waliopewa.
Serikali ya Marekani imekuwa ikifanya marekebisho ya matumizi ya rasilimali zake duniani kwa kupunguza baadhi ya shughuli katika ofisi za balozi.
Athari kwa Waombaji wa Visa
Mabadiliko haya yanamaanisha kuwa wananchi wa nchi ambazo hazitakuwa miongoni mwa vituo 20 vilivyoidhinishwa watalazimika kusafiri hadi nchi nyingine ili kuwasilisha maombi yao ya visa au kuhudhuria mahojiano.
Hali hii inaweza kuongeza gharama za usafiri, malazi na muda wa kusubiri huduma. Kwa baadhi ya waombaji, hususan wale kutoka nchi zenye miundombinu hafifu ya usafiri, hatua hiyo inaweza kuwa changamoto kubwa.
Huduma Zitakazobaki Katika Nchi Zisizo Vituo Rasmi
Ingawa baadhi ya balozi na ofisi za ubalozi hazitashughulikia tena maombi ya visa kwa kiwango kamili, hazitafungwa kabisa. Zitaendelea kutoa huduma kwa raia wa Marekani ikiwemo, uhuishaji wa pasipoti, huduma za dharura za kibalozi, visa za kidiplomasia, kesi maalumu zinazohusiana na maslahi ya taifa la Marekani.
Japo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikufafanua kwa kina mambo mengine yaliyotajwa katika waraka huo, lakini ilisema kuwa inaendelea kutathmini shughuli zake za nje ya nchi ili kuhakikisha rasilimali za walipa kodi wa Marekani zinatumika kwa njia inayotekeleza vipaumbele vya nchi hiyo kwa ufanisi na kwa matokeo bora zaidi. Huku ikieleza kuwa inajumusha mchakato wa visa unaodumisha viwango vya juu vya usalama katika uchunguzi na uhakiki wa waombaji, huku ukilinganisha rasilimali na uwezo wa kiutendaji na maslahi ya taifa la Marekani.
Kwa mujibu wa waraka huo, vituo 20 vitakavyoendelea kutoa huduma zote za visa Afrika ni
- Abidjan, Ivory Coast
- Accra, Ghana
- Addis Ababa, Ethiopia
- Cape Town, Afrika Kusini
- Dakar, Senegal
- Dar es Salaam, Tanzania
- Djibouti, Djibouti
- Johannesburg, Afrika Kusini
- Kampala, Uganda
- Kigali, Rwanda
- Kinshasa, Congo
- Lagos, Nigeria
- Lome, Togo
- Luanda, Angola
- Malabo, Equatorial Guinea
- Monrovia, Liberia
- Nairobi, Kenya
- Port Louis, Mauritius
- Praia, Cape Verde
- Yaounde, Cameroon.
Wachambuzi wa sera za nje za Marekani kwa utawala wa Rais Trump wanaeleza kuwa uamuzi wa nchi hiyo wa kupunguza vituo vya utoaji visa Afrika unaonesha mwelekeo mpya wa sera zake za uhamiaji na usimamizi wa huduma za kibalozi.
Ingawa serikali ya Marekani inaeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi na usalama katika mchakato wa utoaji visa, waombaji wengi barani Afrika wanaweza kukabiliwa na changamoto mpya za usafiri na gharama za ziada.
Kwa sasa, waombaji wa visa wanashauriwa kufuatilia matangazo rasmi kutoka ubalozi wa Marekani katika nchi zao ili kujua jinsi mabadiliko hayo yatakavyowaathiri.

.png)
Post a Comment