MTANGAZAJI

DIT YAKARIBISHA USHIRIKIANO NA SHULE YA SEKONDARI YA KIWANGWA

 


Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Marco Ndomba amesema Taasisi yake iko tayari kushirikiana na Shule ya Sekondari ya Kiwangwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti katika TEHAMA na ukuzaji wa vipaji na ubunifu ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii katika halmashauri ya Chalinze.
 
Prof. Ndomba ameyasema hayo alipotembelea Shule hiyo akiwa ameambatana na baadhi ya wafanyakazi wengine wa DIT kukabidhi vifaa mbalimbali kwa Shule hiyo kufuatia ajali ya moto iliyotokea Julai 22, 2021 na  kuteketeza Bweni la wanafunzi wa Kidato cha Pili na cha nne wapatao 96.
 
Ugeni huo wa DIT ulipokelewa  na Mbunge wa Jimbo la Chalinze  Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni mlezi wa shule hiyo, Diwani wa Kata ya Kiwangwa,viongozi mbalimbali,na wafanyakazi kutoka DIT ambapo walitoa rimu za makaratasi 30 na masweta 40.
 
Ridhiwani amesema ujio wa DIT umeleta matumaini mapya ya kuwatia moyo wanafunzi nakuwafundisha kuona umuhimu wa kurudisha kwa jamii watakapomaliza masomo yao.
 
Amemuomba Mkuu wa Taasisi hiyo kuona ni jinsi gani Taasisi inaweza kuboresha maabara za shule hiyo ili wanafunzi wajifunze kwa njia ya vitendo zaidi badala ya nadharia peke yake. '' vijana wanapenda kujifunza tuwawezeshe kwenye Teknolojia ili kuwaondoa kwenye dhana ya kuolewa ili nao wawe watu muhimu katika jamii'
 
 Katika tukio hili walimu wakike kutoka DIT Idara ya Kompyuta Mwalimu Rachel na Mwalimu Neema kutoka Idara ya Masomo ya Jumla walipata fursa ya kuwahamisisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi na kuwasisitizia juu ya kutokukata tamaa na kuyapenda masomo hayo ili waweze kusoma DIT kozi za Teknolojia.
 
Dada Mkuu kutoka shule ya Sekondari Kiwangwa aliushukuru Uongozi wa DIT kwa kuwatembelea na kuwafariji, na kusema kuwa, ujio huu umewatia moyo na kuahidi kuongeza bidii ili waweze kufanya vizuri ikiwezeka wafungue viwanda Tanzania.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.