MTANGAZAJI

RAIS WA MAREKANI BARACK OBAMA AMWALIKA RAIS JK MAREKANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete yuko njiani kwenda Washington, Marekani kuhudhuria Mkutano wa
Wakuu wa Nchi Tajiri Zaidi na Zenye Viwanda (Group of Eight – G-8) kwa
mwaliko wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Hussein  Obama.

Rais Kikwete na ujumbe wake waliondoka nchini usiku wa jana,Jumanne,

Mei 15, 2012 kwenda Marekani kupitia Nairobi, Kenya na London,
Uingereza.

Rais Kikwete ni mmoja wa Marais wanne wa Afrika ambao Rais Obama

amewaalika kuhudhuria Mkutano wa G-8 ambao unafanyika Jumamosi kwenye
eneo la mapumziko ya marais wa Marekani, Camp David, katika Jimbo la
Maryland.

Hata hivyo, shughuli za kikao hicho zinaanza rasmi leo Mei 17 wakati Waziri

wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton atakapokutana na
viongozi wa nchi wataohudhuria mkutano wa mwaka huu wa G-8.

Mbali na Rais Kikwete, marais wengine wa Afrika walioalikwa na Rais

Obama kuhudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU)
Mheshimiwa Thomas Boni Yayi, Rais wa Ghana Mheshimiwa Atta John Mills
na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Meles Zenawi.

Rais Kikwete amealikwa kushiriki katika mkutano wa mwaka huu wa G-8

ili kutoa uzoefu wake katika mapambano ya kuendeleza kilimo na kuleta
usalama wa chakula katika Tanzania na Afrika kwenye kikao ambacho
kitazungumzia “Hali ya Kilimo Duniani na Usalama wa Chakula” ambacho
Rais Obama atakuwa mwenyekiti wake na ambacho Rais Kikwete atazungumza
kwa dakika 10.

Rais Kikwete amealikwa kwa sababu ya uongozi wake katika masuala ya

maendeleo ya kilimo ambao ameuonyesha kwenye uanzishwaji wa program
mbali mbali hapa nchini na katika Afrika zikiwamo za ASDP
(Agricultural Sector Development Programme), Kilimo Kwanza na SAGCOT
(Ukanda wa Maendeleo ya Kilimo Kusini mwa Tanzania).

Rais Kikwete pia ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioko mbele

katika kuendeleza programu ya kilimo ya Grow Africa Partnership ambako
nchi saba za Afrika zinashirikiana na wadau wa kimataifa kuendeleza
kilimo katika Afrika.

Mkutano huo wa G-8 unafanyika wakati kuna habari za uwezekano wa

kutokea kwa upungufu wa chakula na hata kuzuka kwa baa la njaa katika
baadhi ya nchi za Afrika.

Wakati wa ziara hiyo ya siku tano, Rais Kikwete pia atakutana na

kufanya mazungumzo na maofisa wa Shirika la Millenium Challenge
Corporation (MCC), wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel
Yohanes.

Tanzania ni miongoni mwa washirika wakuu wa MCC, ambacho ni chombo cha

jitihada za maendeleo cha Serikali ya Marekani na ambacho kwa sasa
kinatekeleza miradi mbali mbali ya miundombinu yenye thamani ya dola
za Marekani milioni 698 katika Tanzania.

Katika Marekani, Tanzania inaelezwa kama nchi mfano wa mafanikio

katika utekelezaji wa miradi ya MCC na Rais Kikwete anasifiwa kwa
utekelezaji wa miradi hiyo unaongozwa na uwazi na ufanisi wa kiwango
cha juu.

Imetolewa na:


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.
Dar es Salaam.
16 Mei, 2012

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.