MTANGAZAJI

NIDHAMU YA WANAFUNZI

Ilikuwa ni asubuhi ya aina yake siku ya alhamisi Septemba 24, 2009 ambapo tuliamshwa na mabomu ya Mbagala. Wakati baadhi ya watu walitania kwamba ni salamu za Iddi, wengine walisema huenda ni majaribio ya mabomu yaliyoandaliwa kwa ajili ya kupelekwa Pemba na Unguja kudhibiti fujo wakati wa uandikishaji wa wapiga kura.

Katika harakati za kunusuru maisha, nilifika barabarani na kuparamia daladala chakavu ambalo wala sikujua lilikuwa linaelekea wapi hadi pale lilipopata pancha maeneo ya Mtoni kwa Aziz Ali ndipo nikang’amua kwamba lilikuwa ni basi aina ya DCM lililokuwa likielekea Mwenge. Tulisubiri hapo hadi wazibe pancha maana hata tairi la akiba (spare tyre) hawakuwa nalo. Wakati tukizubaa zubaa na kuulizana kulikoni na abiria wenzangu, alitokea mwanaume mmoja wa umri wa kati akiwa uchi wa mnyama akiwa anaimba, kufoka na kupepesuka. Wenyeji wa hapo walisema wanamfahamu. Ana akili timamu ila tu pombe za sikukuu ya Iddi zilikuwa zimempagawisha. Nyuma yake alifuatwa na msururu wa watoto waliokuwa wakimshangaa na wengine kumcheka.

Wakati wengine tukiendelea kujiaminisha kwamba tulichokiona sio jinamizi, huku wengine wakikejeli kwamba naye alikurupushwa baada ya kusikia mabomu ya Mbagala, walitokea mabaunsa watatu walioshiba ambao, bila hata kuzungumza wala kujali mishangao yetu, walimvuta hadi katikati ya barabara sehemu ambayo magari hayapiti. Bila kupoteza muda, walimtwisha masumbwi kadhaa ya nguvu na akaonekana pombe zimemwishia. Wakati hayo yakiendelea, akatokea muungwana mwingine ambaye pia hatukung’amua alitokea wapi. Yeye alitoa suruali moja chakavu japo iliyofuliwa vizuri. Alimvalisha na, kwa aibu, Bwana yule alianza kuondoka ndipo mimi na abiria wenzangu tulipochangachanga hela na kumnunulia shati la mtumba ili ajisitiri. Alivaa na kuondoka ila hakuna aliyempa pole.

Basi, kama ilivyo kawaida ya watanzania, habari ya mabomu haikuendelea tena. Mazungumzo yote yalilenga kwa huyo jamaa na mabaunsa ambao wala hawakuwa na muda wa kuongea chochote. Wao walimtia adabu na kuondoka zao.“unajua ndugu yangu hiki kizazi hovyo sana. Haya mambo tumezoea kuyaona kwa mabinti zetu wanaotembea nusu uchi kwa kuvaa vimanati [kaptula au sketi fupi] na vishati vya kitovu nje ili kuvutia wanaume wapumbavu wawapatia pesa. Hiyo ni biashara na wao wanafanya hivyo wajipatie pesa; maana wateja wao wanataka hivyo. Sasa huyu mwenzetu tumweleje?” Alisikika abiria mmoja akitamka huku wengine wakimsikiliza kwa makini. Mengi yalizungumzwa na yote yakielekea kuonesha kwamba si kawaida ya mwanaume kuonekana akiwa nusu uchi au kuvaa nguo za aibu kama ilivyo kwa wasichana wa kizazi cha leo.

Hapa ndipo utandawazi ulipotufikisha. Umeua kabisa tamaduni na maadili ya kitanzania kwani kila kinachoonekana kufanywa na mzungu basi ndicho kinachoonekana ni maendeleo. Anayekemea anaitwa mshamba aliyepitwa na wakati. Utakuta watu na akili zao wanatumia pesa kununua madawa ya kulevya. Tunashangazwa kuona mpaka wanaume leo wanajigeuza na kuwa mashoga. Kisa? Wameona mashoga wa kizungu katika runinga na wengine wakipita hapa Bongo na kujitangaza kwamba wao ni mashoga. Kwa mabinti zetu ndio usiseme kabisaa. Akiwa kwao anaitwa Ghati. Akifika mjini tu utakuta anajibadili jina na kuitwa Getrude. Hapo sasa hata nywele anazikarangiza, ngozi anaichubua, anavalia vimanati, anabadili hata namna ya kutembea na anaongelea puani huku akichanganya maneno ya kiingereza na kiswahili makusudi. Utadhani ni mtalii wa kizungu anayejifunza Kiswahili; kumbe katoka kwao Shirati juzi tu. Hata ndege yenyewe inayobeba wazungu hajui hata uwanja wake unafananaje kwani anaiona angani tu. Yote haya anafanya ili aonekane mzungu. Kama hayo ndio maendeleo, hebu na tuendelee hivyo tuone kama kweli tutafanana na hao wazungu kimaendeleo.

Swala hili la mabomu, kadhia ya huyu mlevi, tafrani ya kihistoria iliyofuata pamoja na mazungumzo mafupi yaliyofanywa, yaliifanya kurunzi kumulika yanayotokea katika mashule yetu na namna yanavyochangia katika mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi hasa baada ya kuingia kwa soko huria katika sekta ya elimu. Mijadala mingi imefanyika ambapo lawama nyingi sana zimerushwa kwa wazazi ambao wanawapatia watoto wao uhuru kupita kiasi hadi kufikia kuwapatia pesa za kukodishia mabasi kwenda fukweni na wenzao wa jinsia tofauti, kununua mavazi yasiyofaa, kununua, kusafirisha na/au kutumia madawa ya kulevya, bangi, kununua simu za bei kubwa na kuzitumia katika vitendo vya ufuska na maswala mengine yasiyo ya kimaadili.

Lawama nyingi zimerushwa katika mashule binafsi ambayo yanatuhumiwa kujali zaidi kukusanya pesa kuliko kuangalia nidhamu za wanafunzi. Kama lawama hizi zikinyamaziwa, jamii itachukulia kwamba ni za kweli na matokeo yake ni wazazi kukosa imani na shule binafsi na hivyo kutowaleta vijana wao huko. Ikumbukwe kwamba huu ni muda tete sana ambapo mashule haya yanatoa fomu za kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2010. Kuanza kuzichafulia jina kwa sasa ni sawa na kurusha mabomu mabaya kuliko yale ya Mbagala maana litavuruga azma nzima ya kuwakomboa watanzania kutoka katika makucha ya umaskini na maradhi unaotokana na ujinga ambao sasa umekuwa ni donda ndugu.

Kuchafuliwa majina kwa mashule binafsi ni sawa kabisa na kisa cha mama mmoja aliyemwacha mtoto wake kivulini huku akilindwa na Mbwa wake dhidi ya hatari yoyote wakati yeye akiendelea na palizi ya shamba lake. Mbwa huyu alikuwa ni mwaminifu sana kwani alitokea nyoka aliyetaka kummeza mtoto. Mbwa huyu alipambana naye hadi kumuua. Punde si punde, mama alirudi na kumkuta mbwa wake ametapakaa damu mdomoni huku mtoto akiwa amelala fofofo. Kabla hata hajamuona mtoto wake na, kwa hamaki, mama huyu alidhani kwamba mbwa huyu amemla mtoto wake. Ghafla, bila hata kuchunguza, mama huyu aliinua juu jembe na kumkataka mbwa hadi kufa. Kisa hiki ni sawa kabisa na vita dhidi ya shule binafsi inayoendelea hivi sasa weza kuziua kabisa kama mbwa huyu maskini alivyouawa na yule mama kwa kudhaniwa ameua mtoto kumbe ameua adui wa mtoto yaani nyoka.

Juma lililopita, kurunzi ilimulika sana kwenye shule za kata pamoja na vituo vya tuisheni kama mizizi ya mmomonyoko wa maadili katika jamii. Kwa leo, ni bora tukijiweke sawa ili kwamba sote tumwelewe vizuri “mbwa” wetu mwaminifu (wamiliki wa shule binafsi) na huyu mama (wazazi wanaowaleta watoto wao katika shule binafsi zilizotapakaa damu baada ya kumuua “nyoka” ujinga aliyetaka kumwangamiza mtoto) ili tujue namna ya kupambana na mmonyoko wa maadili badala ya kusubiri madhara mabaya kuliko yale ya mabomu ya Mbagala. Huwezi kujua namna ya kupambana na adui bila ya kumfahamu vizuri. Kwa namna ile ile, unaweza kujikuta unamuua rafiki yako kwa vile tu amechafuliwa jina na ukadhani kwamba huyo ndiye adui.

Kwanza kabisa tuangalie matamko mbalimbali ya kisera yanayohusu falsafa ya elimu, taratibu za usajili na uendeshaji wa shule binafsi, saikolojia ya wamiliki wa shule hizi ikiwa ni pamoja na ya wazazi wanaowaleta vijana wao katika shule hizi. Kwa ujumla wake, falsafa ya elimu tunayoifuata ni ile ya mwaka 1967 yaani elimu ya kujitegemea. Elimu inayotolewa nchini inafuata misingi ya falsafa ya elimu ya kujitegemea. Falsafa hii inatamka kwamba “Elimu ya kujitegemea ina maana ya ujifunzaji wenye manufaa (meaningful learning) katika nyanja zote kuu tatu yaani utambuzi, utendaji na uelekeo. Ujifunzaji wa aina hii unatambuliwa na viashiria (indicators) vifuatavyo: ushirikishaji, uhusishaji wa nadharia na vitendo, uadilifu, kujiamini, kujiendeleza, kuwa na stadi za maisha, ushindani,kuthamini usawa, ujasiriamali, ubunifu, udadisi, uvumbuzi, uwezo wa kuchambua na kutathmini”

Maana ya falsafa hii ni kwamba, shule zote bila kujali kama ni za serikali au binafsi zinatakiwa kumjenga mwanafunzi kimaadili na sio tu kumfanya afaulu mitihani. Kwa kweli, serikali inalisimamia sana hili katika shule binafsi na inahakikisha kwamba kila kilichoandikwa kinafuatwa na shule hizi kikamilifu. Ili kutimiza masharti hayo, wamiliki wa shule hizi huingia gharama kubwa sana katika kuweka miundombinu. Kwa upande wa wazazi, wao huchangia kuhakikisha kwamba mwalimu aliyeajiriwa katika shule hizi ana sifa zote zinazotakiwa yaani taaluma, uchapakazi, kujiheshimu mwenyewe na pia kuwa na uwezo wakusimamia maadili ya wanafunzi anaowaongoza.

Kwa kuzingatia hilo, wamiliki wa shule pamoja na wazazi wanaowaleta wanafunzi katika shule hizi ni watu wa kipato cha kati hadi juu. Watu hawa wanaweza kuwa wasomi, wafanyabiashara au watu wenye mamlaka serikalini, kwenye makampuni au mashirika ya hiari. Haiwezekani mtu akaibuka tu na kujenga shule au kuleta mtoto shule binafsi bila kuwa na uwezo wa kifedha au kuwa na upeo wa kuelewa kwamba maadili ni kiini cha mafanikio ya mwanafunzi kitaaluma. Kwa namna ambavyo serikali inazifuatilia kwa karibu shule binafsi, haitegemewi kabisa kukuta shule yoyote ikiruhusu vitendo vya kuvunja maadili vikifanyika kwa wazi na ikaachwa bila kufutiwa usajili au kukosa wanafunzi kabisa.

Kurunzi inatoa wito kwa watanzania wote wafanye uchambuzi wa kina kabla ya kuzihukumu kimakosa shule hizi ambazo, kwa kweli, ndio mkombozi wa watoto wetu. Kwa upande wa wazazi, tunawaomba muendelee na moyo wenu wa kuzipenda shule hizi. Mnapowaleta watoto wenu huko, tafadhalini jueni kabisa kwamba wako katika mikono salama.maadili yao yatalindwa na watapata taaluma nzuri ili wawe wajenzi wazuri wa Taifa letu la Tanzania.

Mwandishi wa makala hii ni mmiliki wa shule na mshauri wa kujitegemea katika maswala ya usimamizi wa elimu. Pia ni katibu mkuu wa chama cha wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali (TAMONGSCO) na ni mjumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC). Anapatikana kwa namba 0715/54/84-316570 au baruapepe tamongsco@yahoo.com


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.