MTANGAZAJI

EACC KUSHIRIKIANA NA KANISA LA WAADVENTISTA KUPAMBANA NA RUSHWA KENYA.

 


Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa nchini Kenya (EACC) na Kanisa la Waadventista wa Sabato zimeonyesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wao katika kukuza uadilifu, maadili mema na uraia wenye uwajibikaji nchini humo.

Taasisi hizo mbili zilifanya kikao cha mashauriano hivi karibuni kujadili maeneo ya ushirikiano, zikitambua mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kujenga maadili ya jamii na kukuza utamaduni wa uadilifu.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa EACC, Dkt. David Oginde, amesema kuwa rushwa bado ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya Kenya, ukiathiri utoaji wa huduma, kupunguza imani kwa wananchi kwa taasisi za umma na kudhoofisha maadili yanayoiunganisha jamii.

Alisisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa vinahitaji juhudi za pamoja, akibainisha kuwa Kanisa ni mshirika muhimu katika kuhamasisha tabia njema na kukuza maadili miongoni mwa wananchi huku akisisitiza kuwa na waumini wengi na uwepo mkubwa katika jamii mbalimbali kote nchini, alisema Kanisa lina nafasi nzuri ya kuwafikia watu wa rika na mazingira tofauti.

Akiiwakilisha Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa EACC, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Tume hiyo, FCPA John Lolkoloi, alithibitisha tena dhamira ya EACC ya kujenga ushirikiano imara na wenye mfumo rasmi zaidi na taasisi za kidini kupitia vyombo vyao vya kitaifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti  wa Kanisa la Waadventista wa Sabato  katika Unioni Konferensi ya Mashariki mwa Kenya (EKUC), Mchungaji Dkt. Joel Okindo, aliukaribisha ushirikiano huo uliopendekezwa na kueleza utayari wa Kanisa kufanya kazi kwa karibu na Tume katika kukuza uadilifu.

Alisema Kanisa lina hamu kubwa ya kushirikiana katika kuwahamasisha na kuwalea vijana kuwa raia wenye uwajibikaji, likijenga juu ya programu zake zilizopo za malezi na ushauri kwa vijana.

Maeneo yaliyopendekezwa ya ushirikiano ni pamoja na kuwawezesha vijana kuwa mabalozi wa uadilifu, kukuza uraia wenye uwajibikaji, kuwajengea viongozi wa dini maarifa na uwezo wa kuhimiza uwajibikaji na uongozi wa maadili, pamoja na kuhamasisha mijadala ya kijamii kuhusu uadilifu na utawala bora.

Ushirikiano huu ni sehemu ya juhudi za EACC za kujenga ushirikiano na taasisi za kidini katika mapambano dhidi ya rushwa.  EACC imekuwa na mazungumzo na ushirikiano na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB), Muungano wa Makanisa ya Kiinjili Kenya (EAK) na Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kenya (NCCK).

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.