MTANGAZAJI

UDA KENYA YASOGEZA UCHAGUZI KWA AJILI YA WAADVENTISTA

 


Chama tawala cha Kenya, United Democratic Alliance (UDA), kimebadilisha ratiba ya uchaguzi wa maafisa wa ngazi ya wadi katika kaunti za Kisii na Nandi ili kuwapa nafasi Waadventista wa Sabato. 

Uchaguzi huo, ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika Jumamosi ya Oktoba 3, sasa utafanyika Ijumaa, Oktoba 2, mwaka huu kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni, kwa mujibu taarifa ya Septemba 12 kutoka Bodi ya Uchaguzi ya Taifa ya chama hicho iliyoripotiwa na gazeti la People Daily na kwenye mtandao wa X kupitia account yake rasmi.

 Uchaguzi katika kaunti nyingine 11 za awamu hiyo utaendelea kufanyika Jumamosi kama ilivyopangwa. Ripoti kutoka The Star ilithibitisha kuwa UDA awali ilikuwa imepanga Kisii na Nandi miongoni mwa kaunti 13 kupiga kura Oktoba 3.

“Kwa kuzingatia ibada ya kidini ya waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato katika kaunti za Kisii na Nandi,” bodi ilisema, imeamua kubadilisha tarehe ya uchaguzi. Mabadiliko hayo yanawahusu maafisa wa chama wanaotafuta nafasi za uongozi wa wadi pamoja na wanachama wengine wanaoshiriki katika mchakato huo. UDA inaendesha uchaguzi huu kama sehemu ya juhudi pana za kuimarisha uongozi wake wa ngazi za chini kuelekea uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2027.

Kisii ni mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa ya Waadventista nchini Kenya. Kwa mujibu wa Adventist Yearbook, Konferensi ya Kenya Kusini, inayojumuisha sehemu kubwa ya Kaunti ya Kisii, inaripoti takribani waumini 112,000 katika makanisa 444. Eneo jirani la Field ya Kusini Mashariki ya Kanisa la Waadventista linalohusisha sehemu ya Kisii, linajumuisha zaidi ya waumini wa kanisa hilo 108,000. Mabadiliko haya yanawawezesha Waadventista wanaoshiriki uchaguzi wa chama hicho kufanya hivyo bila kukiuka utunzaji wao wa Sabato ambayo ni siku ya kuabudu.

 Kanisa la Waadventista wa Sabato halikatazi washiriki wake kushiriki chaguzi za kisiasa ingawa linawahimiza ushiriki wa uwajibikaji, uhuru wa dhamiri, na kuepuka mgawanyiko wa kisiasa ndani ya kanisa, huku likiweka miongozo ya makanisa kujiepusha na kampeni za kisiasa, kuunga mkono wagombea, kuendesha siasa ndani ya ibada au majukwaa ya kanisa. Hii ikilenga kulinda umoja wa kanisa, kwa sababu waumini wanatoka katika mitazamo na vyama tofauti.

 

 



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.