MTANGAZAJI

POLISI WAELEZA SABABU ZA KUMCHUNGUZA MCHUNGAJI MSTAAFU


 

 

Uchunguzi unaoendelea dhidi ya Mchungaji mstaafu John Bridges (86) unatokana na matokeo mapya ya uchunguzi wa kitabibu na kisayansi yaliyobadilisha uamuzi wa awali kuhusu vifo vya wake zake wawili. 

Kifo cha Joyce (1972) na cha Astrid (1993) kilionekana mwanzoni kuwa ajali, lakini uchunguzi wa kisasa umebaini kuwa vyote vilikuwa mauaji. Kesi hizi zimeunganishwa kwa sababu ya mfumo unaojirudia,wake wawili waliokufa kwa tofauti ya miongo kadhaa, vifo vyote viwili viliripotiwa na Bridges kama “aliwakuta hawajitambui,” vyote vilitangazwa kuwa ajali, na baadaye vyote vimebadilishwa rasmi kuwa mauaji. 

Hali hii imefanya polisi wa Kentucky na Oregon nchini Marekani kushirikiana kwa karibu katika uchunguzi. Zaidi ya hapo, Bridges ameoa mara tano na wake wanne tayari wamefariki, ingawa ni vifo vya Joyce na Astrid pekee vilivyotambuliwa kuwa mauaji, jambo ambalo limeongeza uzito na maswali katika uchunguzi. 

Uchunguzi wa kisasa umegeuza uamuzi wa zamani wa ajali, na kwamba hali hiyo imetokea mara mbili kwa mtu mmoja umeifanya kesi ichukuliwe kama uchunguzi wa mauaji unaoratibiwa kati ya majimbo mawili, badala ya kuwa visa viwili tofauti. 

Polisi wametambua vifo vya mke wake wa kwanza, Joyce “Mable” Bridges (1972, Louisville), na mke wa pili, Astrid Bridges (1993, Gresham), kuwa mauaji. Vifo vya wake wengine havijatangazwa kuwa mauaji.

Joyce alikufa mwaka 1972 katika tukio lililoonekana kuwa ajali, lakini uchunguzi mpya uliofanywa baada ya mwili wake kufukuliwa mwaka 2015 ulionyesha kuwa aliuawa. Kesi hiyo sasa inachunguzwa na kitengo maalum cha polisi kinachofungua upya na kuchunguza kesi za zamani kwa kutumia mbinu mpya za uchunguzi, teknolojia ya kisasa, au taarifa mpya kutoka kwa umma maarufu "Cold Case" cha Louisville.

Zaidi ya miaka 20 baadaye, mwaka 1993, Astrid alikutwa amekufa nje ya nyumba yao huko Oregon. Kifo chake pia kilionekana kuwa ajali, lakini uchunguzi wa baadaye ulithibitisha kuwa ni mauaji. Polisi wa Gresham wamemtaja Bridges kama mshukiwa katika kifo hicho.

 Polisi wamepekua nyumba ya Bridges huko Missouri na kumhoji, ingawa hajakamatwa wala kushtakiwa. Polisi wanasema hawamchukulii kuwa tishio kwa umma isipokuwa labda kwa mke wake wa sasa.

 Marekani ina utaratibu wa Cold Case ili kuhakikisha kwamba kesi za zamani hazifutwi au kusahaulika, hasa pale ambapo teknolojia mpya au ushahidi mpya unaweza kubadilisha uamuzi wa awali. Badala ya kufunga faili na kuendelea, polisi huweka kesi hizo wazi ili ziweze kufunguliwa upya wakati wowote kunapopatikana taarifa mpya, maendeleo ya kisayansi, au mashahidi wanaojitokeza baada ya miaka mingi. Kwa kuwa mauaji nchini Marekani hayana muda wa mwisho wa kisheria, kesi inaweza kuchunguzwa hata baada ya miongo kadhaa kupita.

 


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.