MTANGAZAJI

VODACOM M-PESA KUWEZESHA PAYPAL NCHINI TANZANIA

 


Vodacom M-PESA Tanzania imeingia ushirikiano na PayPal kuwezesha wateja kuhamisha fedha kati ya pochi za M-PESA na akaunti za PayPal, ikiwa ni juhudi za kuboresha huduma za malipo ya kidijitali ya kuvuka mipaka.

Kwa mujibu wa kampuni hizo, mfumo huo ambao unapatikana kupitia programu ya M-PESA Super App, utawawezesha watumiaji wanaokidhi vigezo kuweka fedha kwenye akaunti zao za PayPal pamoja na kutoa fedha kutoka PayPal na kuziingiza moja kwa moja kwenye pochi zao za M-PESA.

Ushirikiano huo unakuja wakati ambapo mahitaji ya huduma rahisi za malipo ya kimataifa yanaongezeka miongoni mwa Watanzania wanaojihusisha na biashara za kimataifa, kazi za kujitegemea mtandaoni pamoja na huduma za kidijitali.

Kupitia huduma hiyo mpya ya kutoa fedha kutoka PayPal kwenda M-PESA, Watanzania sasa wataweza kupata mapato yao ya kimataifa kwa urahisi zaidi.

Aidha, huduma hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kupanua uwezo wa malipo ya kimataifa ndani ya mfumo wa M-PESA.

Kaimu Mkurugenzi wa M-PESA Vodacom Tanzania, Tulisindo Mlupilo, amesema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kuwaunganisha wateja na fursa zaidi kupitia ubunifu na huduma jumuishi za kifedha.

Amefafanua kuwa Maendeleo ya mawasiliano ya kidijitali yanafungua fursa nyingi zaidi kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa dunia kupitia kazi za kujitegemea, biashara mtandaoni, utengenezaji wa maudhui pamoja na biashara za kuvuka mipaka..

Makamu Mkuu wa Rais na Mkuu wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika wa PayPal, Otto Williams, amesema mfumo huo unalenga kuboresha muingiliano wa huduma za malipo ya kimataifa.

Anasema Duniani kote tunaendelea kushuhudia ukuaji wa biashara za kidijitali na ushiriki wa watu katika kazi za mbali. Kwa kuwezesha uhamishaji rahisi wa fedha kati ya PayPal na M-PESA kupitia kuunganisha akaunti, ushirikiano huu utaleta uzoefu rahisi zaidi wa malipo ya kuvuka mipaka kwa wateja nchini Tanzania.

Watumiaji wataweza kupata huduma hiyo moja kwa moja kupitia M-PESA Super App kwa kuunganisha akaunti zao za PayPal na pochi zao za M-PESA kupitia mfumo maalum wa usajili unaolenga kuhakikisha usalama na urahisi wa miamala kati ya majukwaa hayo mawili.



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.