RITA YATANGAZA BODI YA WADHAMINI MPYA YA KANISA LA WAADVENTISTA TANZANIA
Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini nchini Tanzania (RITA) Bw. Frank Kanyusi ametangaza wajumbe wa Bodi mpya ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini humo huku akiwataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha mali za Kanisa hilo zinalindwa na kutumika kwa maslahi ya waumini wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya RITA ambayo pia imewekwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa RITA na pia kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania Aprili 18 mwaka huu, Kanyusi ametoa agizo hilo wakati wa mafunzo kwa bodi hiyo yaliyofanyika katika ofisi za makau makuu ya RITA jijini Dar es Salaam.
Pia, amewaeleza wajumbe hao kuwa wamepewa dhamana ya kusimamia mali za kanisa hilo kwa niaba ya waumini hivyo wahakikishe wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na kuepuka migogoro na matumizi mabaya ya Madaraka ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa kanisa hilo.
Februari mwaka huu Kabidhi
Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi alitangaza kuivunja Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania kwa alichokieleza kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG kubaini
Bodi hiyo kushindwa kusimamia ipasavyo mali na majukumu yake na hivyo
kutoa siku saba kwa uongozi wa kanisa hilo kuwasilisha majina kumi (10)
ya waumini watakaopendekezwa kuwa wajumbe wapya wa kamati ya mpito
itakayosimamia mali za kanisa hilo hadi itakapopatikana Bodi mpya ya
Wadhamini.
Wajumbe wa Bodi mpya ya wadhamini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato itakuwa na wajumbe sita ambao ni David David Mpwani, Magulilo John Mwakalonge, Mathias Egid Mavanza, Shabatu Nicolaus Msaki, Joseph Fidelis Mngwabi na Enoch Marwa Sando.
Mbali na kupatiwa mafunzo hayo maalum, Bodi hiyo imekabidhiwa vitendea kazi na miongozo ya kisheria ikiwemo Sheria ya Usajili na Usimamizi wa Wadhamini Sura ya 318 , mwongozo wa Katiba na nyaraka nyingine zinazohusu usimamizi wa Bodi za Wadhamini ili ziwe sehemu ya nyezo muhimu zitakazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato, David Mpwani ameishukuru RITA kwa mafunzo hayo na miongozo wanayoendelea kuipata ambayo itawawezesha kitimiza majukumu yao kikamilifu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha mali za kanisa zinalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Post a Comment