MTANGAZAJI

GOOGLE YABORESHA IA KUUNGA MKONO KISWAHILI NA KISOMALI NA LUGHA 11 ZA AFRIKA

 


Google imeongeza wigo wa  zana zake za utafutaji za Muhtasari wa taarifa wa AI unaoitwa AI overviews na AI Mode ili kuunga mkono lugha 13 za Afrika, pamoja na Kiingereza. Maboresho haya yanawawezesha mamilioni ya watumiaji barani Afrika, hasa nchini Kenya na Tanzania, kuchunguza, kujifunza na kuunda maudhui mtandaoni kwa kutumia lugha zao za asili ikiwemo Kiswahili na Kisomali.

Upanuzi huu unajengwa juu ya uwekezaji wa Google katika matumizi ya AI yenye uwajibikaji katika huduma ya utafutaji (Search). Kupitia AI Overviews, sasa watumiaji wa lugha ya kiswahili wa Afrika Mashariki wanaweza kupata muhtasari mfupi uliotengenezwa na AI kuhusu wanachotafuta, pamoja na viungo vya kuaminika vinavyowasaidia kupata maelezo zaidi. AI Mode inaenda hatua zaidi kwa kuruhusu watumiaji kuwasiliana kupitia maandishi, sauti au picha ili kupata majibu ya kina na yaliyobinafsishwa katika lugha wanayoipendelea.

Lugha hizi 13 zilichaguliwa kutokana na matumizi makubwa na yanayoongezeka ya utafutaji mtandaoni barani Afrika, ili kuhakikisha wimbi la kwanza la AI kwa lugha za ndani linafikia jamii zilizo hai katika nchi kama Kenya, Nigeria, Ethiopia na Tanzania. Mpango huu unawasaidia wanafunzi, walimu na wajasiriamali nchini Kenya kuanza kutumia AI moja kwa moja katika kutatua changamoto halisi katika jamii zao, badala ya kusikia tu kuhusu teknolojia hiyo.

 Takwimu zinaonesha kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha ya kwanza au yapili katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, Inakadiriwa kuwa na watumiaji milioni 150 hadi 200 duniani.Kisomali kinazungumzwa sana Somalia, Djibouti, Ethiopia, na Kenya hasa katika jimbo la kaskazini mashariki huku Jumla ya watumiaji wa Kisomali duniani ikiwa ni  takribani milioni  25 hadi 30.

Upanuzi huu pia umetumia maarifa kutoka kwenye mradi wa lugha wa Google unaoitwa Waxal. Mradi huu unachanganya ujifunzaji wa mashine (machine learning), utafiti wa lugha na ushirikiano wa jamii ili kuboresha jinsi zana za AI zinavyoelewa na kuzalisha lugha za Afrika. Jina Waxal linamaanisha “kuzungumza” katika lugha ya Wolof, likionyesha lengo la mradi la kufanya mawasiliano ya kidijitali yawe jumuishi zaidi na yanayolingana na mazingira ya jamii za Afrika.

Kwa pamoja, maboresho haya yanaonyesha dhamira ya muda mrefu ya Google ya kujenga uwezo wa AI kwa lugha za Afrika ambao ni wa kisasa kiteknolojia lakini pia unaozingatia utamaduni wa jamii husika.

Kupanua AI Overviews na AI Mode katika lugha nyingi zinazozungumzwa sana Kusini mwa Jangwa la Sahara ni hatua inayofuata katika kazi hii. Hatua hii inawawezesha wanafunzi, walimu, watafsiri, wajasiriamali na watumiaji wa kawaida kuanza kutumia AI moja kwa moja katika kutatua changamoto zinazowakabili katika jamii zao.

Unaweza kutumia  AI Mode kwa Kiswahili na Kisomali kwa; 

  1. Fungua programu ya Google kwenye kifaa cha Android au iOS (kupitia programu au kivinjari cha simu).

  2. Bofya AI Mode ndani ya huduma ya utafutaji (Search).

  3. Andika au uliza swali kwa sauti katika lugha unayoipendelea, kama Kiswahili au Kisomali.

Google inawaalika watumiaji barani Afrika kujaribu huduma hii, kutoa maoni yao na kusaidia kuboresha jinsi AI inavyofanya kazi katika lugha zao.

Lugha mpya zilizoongezwa ni pamoja na Kiswahili (Kenya, Tanzania), Kisomali (Somalia, Kenya), Kifrikana, Kiakan, Kiamhariki, Kihausa, Kinyarwanda, Kiafaan Oromoo, Kisesotho, Kisetswana, Kiwolof, Kiyorùbá na Kizuru.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.