WAKILI WA HOUSTON MATATANI KWA KUWALAGHAI WAHAMIAJI
Mamlaka za Shirikisho nchini Marekani zimemkamata wakili wa uhamiaji mwenye umri wa miaka 44 kutoka Houston, Texas. Anashtakiwa kwa ulaghai wa kujipatia pesa kupitia barua pepe na kutoa taarifa za uongo.
Alla Nowowiejski alijitokeza kwa mara ya kwanza mbele ya mahakama Jumatano alasiri. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wachunguzi wanasema Nowowiejski alipokea malipo kutoka kwa wateja waliotafuta msaada wa kuanzisha au kurekebisha hadhi yao ya uhamiaji na kuomba vibali vya kazi, ambapo anadaiwa kutowasilisha maombi au aliwasilisha sehemu tu ya maombi hayo.
Hati ya mashtaka inaeleza kwamba Nowowiejski aliwapa wateja nyaraka za kughushi na namba za rejea za kesi ambazo hazikuhusiana na maombi yao, hali iliyowafanya waamini kuwa maombi yao yalikuwa yanashughulikiwa. Akipatikana na hatia, Nowowiejski anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani na faini ya hadi dola 250,000.
Uchunguzi huo uliendeshwa na ofisi za wakaguzi wakuu wa Idara ya Usalama wa Ndani (DHS), Huduma ya Posta ya Marekani, Idara ya Uraia na Uhamiaji (USCIS), na Ofisi ya Polisi wa Kaunti ya Harris.
Takwimu za Mamlaka ya shirikisho zinaonesha matukio ya udanganyifu unaofanywa na mawakili wa uhamiaji yamekuwa yakiongezeka, hasa katika jimbo la Texas. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Texas imekuwa kitovu cha uchunguzi wa makosa ya uhamiaji, huku wilaya za Kusini na Magharibi zikiripoti zaidi ya kesi elfu ishirini na tano za uhalifu wa uhamiaji mwaka 2025 pekee.
Mojawapo ya matukio makubwa zaidi lilihusisha mtu aliyedai kuwa wakili wa uhamiaji na kuwalaghai zaidi ya wahamiaji 100, akikusanya zaidi ya dola milioni moja na nusu kabla ya kukamatwa.
DHS, USCIS na FBI zinasema ongezeko la maombi ya uhamiaji limekuwa likivutia matapeli wanaowatoza waombaji kati ya dola elfu saba hadi kumi na tano kwa maombi yasiyowasilishwa, na kwamba uchunguzi wa makosa ya aina hii umeongezeka kwa kasi huko Texas na majimbo mengine yenye idadi kubwa ya wahamiaji.

Post a Comment